Tuesday, April 27, 2021

KAMATI YA MAKATIBU WAKUU YAANDAA MKAKATI KABAMBE WA KUBORESHA MICHEZO MASHULENI

 


Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye dhamana yaElimu,Michezo na TAMISEMI  wakiwa kwenye kikao kazi leo Aprili 27,2021 Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa masuala mbalimbali ya uimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari hapa nchini chini ya uenyekiti wa Prof.Riziki Shemdoe ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya  TAMISEMI.


Dkt. Hasssan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia eneo la Elimu ndugu  Gerard Mweli (kulia) wakihudhuria kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye dhamana ya Elimu, Michezo na TAMISEMI  wamefanya kikao kazi leoAprili 27,2021Jijini Dodoma kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa masuala mbalimbali  yauimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari hapa nchini. Upande wa pili ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusufu Omary Singo

 

Na John Mapepele, Dodoma

Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zenye  dhamana ya Elimu, Michezo na TAMISEMI  wamefanya kikao kazi leo Aprili 27,2021 Jijini Dodoma kujadili  utekelezaji wa maelekezo ya Mawaziri  wenye dhamana hizo hizo kwa lengo la   kuandaa  Mkakati  wa Utekelezaji wa masuala  mbalimbali  ya uimarishaji wa somo la Elimu kwa Michezo na Michezo katika shule za Msingi na Sekondari  hapa nchini

Mwenyekiti wa Kikao hicho, Prof. Riziki  Shemdoe  ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI amesema  miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa  na kukamilika ni pamoja na   kuandaliwa kwa  mapendekezo ya uimarishaji wa ufundishaji wa somo la michezo shuleni na tahasusi zenye somo hilo kwa kidato cha tano  ambapo ameseme tahasusi hizo zitaanza kufundishwa katika mwaka huu wa masomo.

Pia rasimu ya Mpango Mkakati na Mikakati ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya  somo  la Elimu kwa michezo na michezo katika shule za Msingi na Sekondari  imeandaliwa ili  kuboresha  michezo mashuleni.

Kuhusu kuandaa kiunzi cha uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA  Prof. Shemdoe amesema  tayari  Kamati ya Wataalam imeshauri kuwa  kwa sasa  miongozo iliyopo itumike na kiunzi tayari kimeshaandaliwa kwa kuzingatia changamoto  zilizopo ambapo  kitajadiliwa  na wadau wote Juni mwaka huu wakati wa michezo ya UMISHUMTA NA UMISSETA na  kwa sasa tayari miongozo hiyo imeshatumwa kwenye  mikoa yote hapa nchini.

Aidha, suala la uundwaji wa Kamati ya kitaifa ya UMISHUMTA NA UMISSETA tayari imependekezwa na kukubalika kuundwa kwa Kamati ya Usimamizi itakayoundwa na wataalam wawili wawili kutoka kwenye kila Wizara ambapo imekubalika kuwa  pamoja na usimamizi, Kamati itatumia fursa hiyo kujifunza na kuangalia changamoto zilizopo kwenye uendeshaji wa michezo ya UMITASHUMTA  na UMISSETA kuandaa  mapendekezo yatakayojadiliwa  na wadau wote kwa ajili ya  maboresho zaidi.

Prof. Shemdoe amesema kuhusu mchakato wa maandalizi ya UMISHUMTA NA UMISSETA mwaka huu, tayari mikoa yote imeshaandikiwa barua ya taarifa na Mhe. Waziri Ofisi ya Rais –TAMISEMI na kwamba waratibu wa michezo wanakwenda kwenye ukaguzi wa viwanja na maeneo ya malazi na chakula kuanzia Aprili 28-30, mwaka huu. Pia Kamati ya wataalam inaendelea na ufuatiliaji wa Shule teule za michezo ili kuhakikisha kuwa michezo inafanyika kwenye kiwango kinachotakiwa.

Makatibu Wakuu walioshiriki  kwenye  kikao hiki ni pamoja Mwenyekiti wa kikao hicho, Prof. Riziki  Shemdoe  ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI,na Naibu wake  anayeshughulikia eneo la Elimu ndugu  Gerard Mweli, mwingine ni  Dkt. Hasssan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Dkt. Leonard Akwilapo  kutoka  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojioa pamoja na Watendaji mbalimbali kutoka  Wizara hizo.

Maelekezo  ya Mawaziri wenye dhamana ya elimu, Michezo na TAMISEMI yalitolewa wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika Februari 8, Mwaka huu.

Tuesday, April 20, 2021

SERIKALI YAANZISHA KITUO CHA KIMATAIFA CHA KUENDELEZA VIPAJI VYA MICHEZO.

 


 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omari (kushoto), akiwa naa liyewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na Kocha wa Timu ya Taifa Stars, Ami Ninje (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt. Richard Masika wakikagua eneo la chuo kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa chuo hicho ili kujenga Kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo.

Timu ya wataalam mbalimbali wa michezo na ardhi ikipitia ramani ya maeneo ya ujenzi wa madarasa na hosteli.

Timu ya wataalam ikiangalia eneo la ujenzi wa madarasa wa Kituo cha kuendeleza vipaji vya Michezo

 



Na John Mapepele, Dodoma

 

Serikali inatekeleza mradi wa  kupanua eneo la  Chuo cha  Maendeleo ya Michezo Malya ikiwa ni  mkakati  maalum wa kuanzisha Kituo cha Kuendeleza Vipaji vya Michezo  ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo hapa nchini.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omary ameyasema haya  wakati alipokuwa na  Timu ya wataalam walipotembelea na kukagua eneo  hilo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na hadhi ya kimataifa.

 

“Niseme tu kwamba  kukamilika kwa kituo  hiki kutaifanya  nchi yetu kusonga mbele kwenye  Sekta ya Michezo kwa kuwa  vipaji vya wanamichezo wetu vitaibuliwa na  tutaweza sasa  kushindana  na mataifa mengine duniani sasa” amefafanua Mkurugenzi Omary

 

Amesema Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji kilichokuwa kinakosekana ni kituo maalum cha michezo cha kuwanoa wachezaji na kwamba kukamilika kwa kituo hiki ni suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

 

Awali, Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema  Wizara imeendelea  kufanya mageuzi makubwa ili kutimiza ahadi  za Serikali na matarajio ya wananchi kwa ujumla.

 

Amesema Wizara  inatekeleza kwa kwa kasi  masuala yote  yaliyobainishwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka  2020-2025 ikiwemo ibara125(a)-(h) kwa Sekta ya Habari, ibara239 (a)-(m) kwa Sekta ya Utamaduni, ibara 249 (a)-(j) Sekta ya Sanaa na ibara 243(a)-(k) kwa Sekta ya Michezo.

 

Akihutubia kwenye kikao cha Wafanyakazi wa wa Wizara hiyo hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema tayari Wizara yake imeshakamilisha agizo la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ikiwa pia ni mkakati wa kukuza sekta ya Michezo nchini.

 

“Wizara imekamilisha agizo hili kwa kuhuisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambao umetengewa shilingi bilioni 1.5. 

Mfuko  huu kwa  mwaka ujao wa fedha utajikita katika ujenzi wa miuondombinu muhimu ikiwemo jengo la SANAA HOUSE hapa Dodoma, pia utaendelea  kutengewa fedha zaidi kwa lengo la kutekeleza  majukumu mawili adhimu; kuwajengea uwezo wanatasnia hizo za Sanaa na Utamaduni kupitia mafunzo na  kuwawezesha kupata mikopo na ruzuku katika kazi zao” amesisitiza Waziri Bashungwa

Wednesday, April 14, 2021

MAWAZIRI WATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA SULUHU KIKAMILIFU

 


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul (kushoto) akizungumza leo katika kikao cha Mawaziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Wizara hiyo cha kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Sekta hizo ya kisera, kisheria na kikanuni kwenye masuala ya mawasiliano nchini kilichofanyika jijini Dodoma, anayefuata ni Waziri wake Innocent Bashungwa akifuatiwa na Waziri waMawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile na kuliani Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew.

Kikao hicho kimefanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mheshimiwa  SamiaSuluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  yakutaka kufanyika marekebisho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia Vyombovya Habari  hapa nchini hususan Televishen Mtandao (Online TV)

 

Wajumbe wa kikao cha Mawaziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja naWizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas akizungumza katika kikao hicho cha kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu yaSekta hizo ya kisera, kisheria  na kikanuni kwenye masuala ya mawasiliano nchini kilichofanyika jijini Dodoma leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas (kushoto), akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula akifuatiwa na Naibu wake Dkt. Jim Yonaz katika kikao cha Mawaziri wa Wizara hizo mbili cha kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Sekta hizo ya kisera, kisheria na kikanuni kwenye masuala ya mawasiliano nchin ikilichofanyika jijini Dodoma leo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbas (kushoto) akizungumza leo katika kikao cha Mawaziri wa Wizara hiyo na Wizara ya Mawasiliano naTeknolojiaya Habari cha kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Sekta hizo yakisera, kisheria na kikanuni kwenye masuala ya mawasiliano nchini kilichofanyika jijini Dodoma.Kulia ni Katibu Mkuu waWizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula. Kikao hicho kimefanyika kufuatia maelekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Mheshimiwa SamiaSuluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yakutaka kufanyika marekebisho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia Vyombo vya Habari hapa nchini hususani Televishen Mtandao (Online TV)

 

Na John Mapepele, Dodoma

Waziri anayesimamia Sekta ya Habari Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri anayesimamia Sekta ya Mawasiliano Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na timu ya Makatibu  Wakuu na Wataalam  wa Wizara hizo  wamekaa na kujadili  hoja mbalimbali kuhusu  utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za kisekta kufuatia  maelekezo  ya hivi karibuni ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maelekezo hayo aliyatoa   wakati wa  kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu  Makatibu  Wakuu na  Wakuu wa Taasisi ya kufanya marekebisho ya Sheria na Kanuni  zinazosimamia Vyombo vya Habari hususan Televisheni Mtandao (Online TV).

Majadiliano hayo yamefanyika jijini Dodoma Aprili 14, 2021 na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kwenye hoja 13 zilizoainishwa na Wizara hizo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa  amesema miongoni mwa  maazimio  yaliyofikiwa ni pamoja na kufanya  mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo katika maeneo yote yenye mapungufu  ili ziendane na  hali halisi ya sasa  na  kuweka  mifumo rafiki ya kushughulikia masuala  yote  yanayohusu sekta ya  Mawasiliano na Utangazaji

“Tumeagiza Wataalam wafanye uchambuzi wa Kanuni za Maudhui Mtandaoni ili kuona kama zinaendana na mazingira ya sasa” amesisitiza Waziri Bashungwa

Ameongeza kuwa Wizara zimeaazimia kuja na mkakati wa kuwaelimisha  wadau wa Sekta hizo ili kudhibiti makosa  ya kimaudhui  yanayofanywa  na Vyombo vya Habari badala ya hali ilivyo sasa inayotoa adhabu kali zinazojikita kwenye utozaji wa faini kubwa pamoja na kufungiwa.

Suala lingine ambalo limeazimiwa kufanyiwa kazi ni chaneli za bure kutoonekana kwenye visimbusi ambavyo kimsingi zinapaswa kuonekana hata pale kifurushi kinapokuwa kimeisha muda wake.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine  Ndugulile amesema kukua kwa teknolojia kumewezesha kukua kwa matumizi ya huduma za mawasiliano yakiwemo ya utangazaji hivyo katika kipindi kifupi  kijacho Serikali  kupitia  Wizara hizo mbili  itafanya  maboresho  makubwa  kwenye kanuni husika ili kuendana na  hali halisi ya sasa.

 

Ameongeza kuwa Serikali ilitunga Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali zikiwemo Sheria ya huduma za Habari Namba 12 ya mwaka 2016, Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 na Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambazo pamoja na mambo mengine zinaelekeza kuweka mazingira wezeshi ya kukuza maudhui ya ndani (Local content).

Thursday, April 8, 2021

MHE GEKUL AOMBA USHIRIKIANO BAINA YA VIONGOZI WAKUU WA WIZARA,WATENDAJI NA WATUMISHI

 


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Mhe.Innocent Bashungwa (katikati mwenye tai nyekundu) akiwa  na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Hassan
Abbasi (mwenye tai ya bluu) wakimkaribisha Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul
alipowasili rasmi kwenye Ofisi yake mpya iliyopo eneo la Mji wa Serikali
–Mtumba jijini Dodoma leo, baada ya kuapishwa
na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Pauline Gekul akipokea maua kutoka  kwa
wafanyakazi wa Wizara hiyo  kama ishara
ya kumkaribisha rasmi kwenye Ofisi yake mpya iliyopo  eneo la Mji wa Serikali –Mtumba jijini Dodoma
leo, baada ya kuapishwa  na Mhe.Rais
Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo

a.    Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Pauline Gekul akisaini
kitabu  cha wageni  mara baada ya
kuingia kwenye Ofisi yake mpya iliyopo eneo la Mji wa Serikali –Mtumba
jijini Dodoma leo, baada ya kuapishwa  na
Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo.

Na John Mapepele, Dodoma


Naibu
Waziri wa Habari Utamaduni na Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Philipo
Gekul ameomba ushirikiano baina Viongozi Wakuu wa Wizara, Watendaji na
Watumishi wote wa Wizara ili kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo
kimamilifu kulingana na Miongozo ya Serikali, Maelekezo ya Mheshimiwa
Rais na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hatimaye matarajio ya
wananchi yaweze kufikiwa.

Mhe.
Gekul ameyasema haya alipowasili rasmi leo kwenye Ofisi yake mpya eneo
la Mji wa Serikali- Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kuteuliwa na
Mheshimiwa Rais kwenye nafasi hiyo hivi karibuni akitokea Wizara ya
Mifugo na Uvuvi ambako alikuwa akihudumu kwa nafasi hiyohiyo.

“Mheshimiwa
Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara, madaraka haya
tuliyopewa ni sawa na makoti ya kuazima hivyo tuna kila sababu ya
kumtanguliza Mungu na kuimarisha ushirikiano ili kuleta matokeo
tarajiwa kwa wananchi wetu wakati tunatekeleza majukumu yetu ya kila
siku” amesisitiza Mhe. Gekul

Amemshukuru Mheshimiwa Mama Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na
kumrejesha tena kwenye nafasi hiyo pamoja na viongozi wote Wakuu wa
Wizara hiyo ambapo ameongeza kuwa hali hiyo itarahisisha utekelezaji wa
majukumu ya Wizara kwa ufanisi kwa kuwa watendaji wote wamerejeshwa
na wanauzoefu wa kutosha.

Amemhakikishia Waziri Bashungwa
kufanya kazi kwa bidii ya kumshauri na kumsaidia kwa kadiri ya uwezo
wake wote kama msaidizi wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Watumishi
wote kuwa na mshikamano wa hali ya juu ambapo amesisitiza watumishi
wasisubiri kusukumwa na Katibu Mkuu na badala yake wachape kazi ili
kukidhi dhamira ya Mhe. Rais ya kuwatumikiwa wananchi kikamilifu.

“Napenda
kusema tukigundua mahali popote kwenye Wizara yetu hakuna ushirikiano
tutachukua hatua mara moja maana hiyo itakuwa ni hujuma kwa
taifa”amefafanua Mhe. Bashungwa

Amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa
kumwamini na kumteua tena kuendelea kusimamia Sekta zilizo chini ya
Wizara hiyo pia kumteua Mhe. Gekul kuja kuongeza nguvu katika kutekeleza
na kumuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutekeleza
Ilani ya CCM na hotuba aliyoitoa awali kama mwongozo kwa Watendaji
wote wa Serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi
amemshukuru Mhe.Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua
kwa mara nyingine kuwa Katibu Mkuu na kumwahidi kushirikiana na
Viongozi na Watumishi wote kutekeleza majukumu ya Wizara kwa weledi
na kuzingatia taaluma.

Akizungumza kwenye Kikao cha Menejimenti
ya Wizara hiyo mara baada ya kupokea maelekezo ya Waziri Bashungwa, Dkt.
Abbasi amesisitiza watendaji wa Wizara kutoka na kuwa jirani na wadau
wa sekta zilizochini ya Wizara hiyo kwa kuwa wanahitaji kulelewa kwa
karibu.

Amesema jukumu la Wizara ni kuzisimamia sekta zilizo
chini ya wizara hiyo kikamilifu kwa weledi ili kupata matokeo chanya
kwa kuwa nchi yetu imebahatika kuwa na wasanioi wenye vipaji na vipawa
vingi kinachotakiwa ni usimamizi madhubuti