Thursday, August 6, 2020

NANENANE DODOMA KUANZISHA MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII WA MIFUGO

 

Mwakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, ambaye  pia ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda akijaribu  kuendesha Trekta kwenye maonesho hayo  leo, aliye pembeni yake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel,  walio chini  mwenye miwani ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Injinia Jackson Masaka wakishuhudia tukio hilo. Picha na John Mapepele
Mfugaji wa Mifugo Juma Seleman kutoka  Mpwapwa akipitisha Ng’ombe wake  Mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Viongozi kutoka Mkoa wa Dodoma na Singida  pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa  mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati,ambaye ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda(mwenye kilemba) akimuuliza maswali muoneshaji wa kampuni la uzalishaji wa chakula cha mifugo ya Harsho Group, Juma Ally (mwenye Tisheti ya Njano) Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Anjelina Lutambi. Picha na John Mapepele

Na John mapepele, Dodoma

Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii  kuyafanya mashindano maalum ya Paredi ya Mifugo yanayofanyika kila mwaka kwenye  kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni  jijini Dodoma kuwa Maonesho ya Kimataifa  ya utalii wa mifugo ili kuongeza pato la taifa na kuleta hamasa kwa wananchi kushiriki.

Katika hotuba iliyotolewa kwenye Paredi la Mifugo leo na Mkuu ya Wilaya ya Bahi Mwanahamisi  Athuman Mukunda kwa niaba ya Wakuu hao wa Mikoa, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa nchi ya pili  kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika  hiyo uanzishaji uboreshaji wa Paredi  la mifugo utasaidia  kuinua uchumi wa taifa kwa kuongeza  kipato kutoka kwa watalii  kupitia mifugo.

Ameongeza kuwa jiografia ya Dodoma kuwa katika ya nchi na  hali ya hewa nzuri ya majira ya mwezi Agosti katika eneo la Nzuguni  linafanya watalii wengi kuja kutembelea maonesho hayo.

“Ndugu zangu  niwaambie ukweli  katika nchi yetu miongoni mwa Wizara mama ambazo ni nguzo na tegemeo wa maisha ya wananchi wake na ambayo inaweza kuongeza mapato ya Serikali ni  Wizara ya Mifugo na Uvuvi”  alisisitiza Mhe. Mukunda

Amesema mifugo na uvuvi ni dhahabu inayotembea ambayo kama  itatunzwa  kwa kuzingatia ushauri na utaalam  utaongeza tija na kulifanya taifa lisonge  mbele  kiuchumi

Hata hivyo amesema changamoto inayosababisha kutokuwa na mageuzi ya haraka kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini ni kukosekana kwa wataalam kwenye  ngazi za chini kwa wananchi ambapo amesisitiza kuwa  kuna umuhimu Wizara husika kushusha wataalam hadi kwenye ngazi za vijiji  badala yahali ilivyo sasa ambapo wataalam  wapo kwenye ngazi za juu jambo ambalo linafanya utalaamu usiwafikie wananchi kama ilivyokusudiwa.

Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya Wizara husika kuboresha ushirikiano katika utekelezaji  na utoaji wa maelekezo ambapo amesema  kumekuwa na ushahidi kuwa sehemu ambazo wizara zimeshirikiana kikamilifu na Halmashauri husika kumekuwa na matokeo chanya.

 Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi amepongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo ameelekeza  Halmashauri za Mkoa wa Singida kutenga maeneo  kwa ajili ya kulima malisho ya  mifugo na ameishukuru Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ikungi kuanzisha shamba darasa  bora la malisho ya mifugo ambalo ni la mfano hapa nchini.

“Ukiona Mheshimiwa, Rais Dkt. John Magufuli anawekeza kwenye miradi kama ule wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere Rufiji, Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupola ya Singida lengo ni kujenga uchumi jumuishi” ameongeza Dkt. Lutambi

Amesema Mkoa wa Singida umendelea kupiga hatua katika kutekeleza   miradi mbalimbali ambapo amesema licha ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye zao la Korosho   pia wamesimamia  vizuri sekta nyingine  kama vile  sekta ya madini ambapo muelekeo wa sekta ya madini ni kuwafanya wananchi wamiliki raslimali hii kwa kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amesema  Serikali  ya awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa  kwenye sekta ya mifugo ambapo  viwanda vingi vya nyama  vimeanzishwa, kuboresha kwa miundombinu ya mifugo kama majosho na kuimarisha  minada, kuzuia utoroshaji wa  mifugo kwenda nchi jirani na  kuanza  kutengeneza  chanjo za mifugo ambapo hadi sasa chanjo sita zimekamilika na  nyingine saba zinatarajia kukamilika katika kipindi  kifupi kijacho na kufanya  chanjo  dhidi ya magonjwa 13 za kipaombele kukamilika.

Aidha, amesema Wizara  ya Mifugo tayari imeshatangaza  rasmi tarehe 13/5/2020  bei elekezi za chanjo za wanyama dhidi ya magonjwa 13 ya kipaombele  kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 za Mwaka  2020 kifungu cha 3(2)(g) na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji Na 180 za Mwaka 2020 Kifungu cha 14(b) na (c)  ambapo bei ya dukani nay a kuchanjia kwa dozi  haitazidi  viwango vilivyoainishwa.

Tuesday, August 4, 2020

MAONYESHO YA NANE NANE KANDA YA KATI DODOMA YAING’ARISHA TANZANIA DUNIANI

Waziri wa TAMISEMI,
Mhe. Seleman Jaffo akipokewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt.
Anjelina Lutambi  mara baada ya kuwasili
kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane
kanda ya kati Dodoma leo.kushoto
ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi. (picha na  John mapepele)

   Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti
nyeusi na tai)  akiwa na viongozi wakuu
wa Mkoa wa Dodoma na Singida akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa maonesho
ya Nanenane kanda ya Kati Dodoma kwenye viwanja vya Nzuguni leo. (Picha na John
Mapepele)
    Mkuu
wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ( mwenye kilemba)
akishiriki kucheza Ngoma za Utamaduni za kikundi cha Chuo Kikuu cha
Dodoma wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati
Dodoma wakati Mgeni rasmi Mheshimiwa Seleman Jaffo Waziri wa TAMISEMI
(mwenye suti) akikagua vikundi hivyo. (picha na John Mapepele)

1Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti
nyeusi na tai) akiwa  na viongozi wakuu
wa Mkoa wa Singida na Dodoma  wakipata maelezo
ya kilimo cha mtama kutoka kwa mtaalam wa Wizara ya Kilimo kwenye  viwanja vya Nzuguni -Dodoma wakati wa
ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati.(Picha  na John Mapepele)

       Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti
nyeusi na tai) akipata  maelezo ya
uhimilishaji wa mifugo kutoka kwa mtaalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, nyuma
ni Mwnyekiti wa Maonesho ya Nanenane kanda ya kati, Mhe. Dkt Binilithi Mahenge
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kushoto ni Bi. Aziza Mumba Katibu wa Kamati ya
Maandalizi. (Picha na John Mapepele)

……………………………………………………………..

Na .John Mapepele

Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuanzisha Maonesho ya Nanenane Kanda ya
Kati Dodoma yameufanya Mkoa wa Singida kubuni na kuanzisha kilimo cha
pamoja cha Korosho, zaidi ya ekari 25000 za pamoja.

Hatua
hiyo imelifanya  eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya kilimo
hicho duniani ambalo litasaidia kuipaisha Tanzania katika uchumi wa kati
wa juu na kuwa eneo maarufu la utalii wa kilimo duniani.

Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti Mwenza wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati
Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida kwenye
ufunguzi rasmi wa maonesho hayo kwa mwaka huu.

Maonesho
hayo ya kanda ya kati katika viwanja vya maonesho vya Nzuguni jijini
Dodoma wakati akitoa salamu za Mkoa huo kabla ya kumkaribisha
Mwenyekiti wa Kanda ya Kati Mhe, Dkt. Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma ili amkaribishe Mgeni Rasmi wa Maonesho hayo Mhe.
Selemani Said Jaffo, Waziri wa TAMISEMI

Dkt. Nchimbi amesema
elimu iliyotolewa na taasisi mbalimbali za kilimo kwenye maonesho hayo
ziliufanya mkoa uweze kuanzisha mashamba hayo makubwa kwenye Wilaya
ya Manyoni, Ikungi na Itigi baada ya kupata msaada wa kitaalamu kutoka
Bodi ya Korosho nchini na Watafiti kutoka chuo cha Kilimo cha
Naliandele ambao wamefungua ofisi baada ya kuona kuwa kuna uhitaji wa
kipekee wa kuwa hapo kutokana na tija kubwa ya zao hilo katika Mkoa wa
Singida.

“ Kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na mashamba
makubwa ya Korosho natoa wito kwa wawekezaji wa viwanda vya kubangua
Korosho kuja Singida ili kuwekeza kwani kutakuwa na malighafi ya
kutosha na ya uhakika katika kipindi kifupi kijacho” alisisitiza Dkt.
Nchimbi.

Ameongeza kuwa utafiti uliofanyika umeonesha Korosho za
Singida zinauwezo wa kuzaa mara mbili kwenye msimu mmoja kutokana na
hali ya hewa katika eneo hili na kwamba mkulima mmoja tayari
amepata kilo 100 kutoka kwenye mkorosho mmoja kwa mwaka mmoja tu hali
ambayo inaashiria zao hilo lina tija kubwa kwa wakulima.

Amesema
kwa sasa Mkoa wa Singida unahamasisha “Nanenane Kaya” kwa maana ya
kuwa kila kaya lazima kuzingatia maarifa yanatolewa na wataalam
kwenye maonesho ya nanenane kanda ya katika maeneo ya kilimo, mifugo
na uvuvi ili kuongeza kipato.

Ameongeza kuwa kwa sasa mkoa
unajipanga kuongeza zao la Parachichi ambapo amesema tafiti zinaonyesha
kuwa ardhi ya Mkoa wa Singida inafaa kwa kilimo cha zao hilo na kwamba
kinachotakiwa ni kupata maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji wa
zao hilo.

Ampongeza  Rais John Pombe Magufuli kwa kuiingiza
Tanzania kwenye uchumi wa Kati na kuwaomba watanzania kumchagua tena
katika kipindi kijacho ili maono yake ya kuhakikisha uchumi wa nchi
unakua kwa kasi itimie.

“Kwa
mkoa wa Singida tumejipanga kuhakikisha tunaunga mkono jitihada hizo
kwa kufanya kazi kwa bidii na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji
katika mkoa huo”Alisema 

Awali akizungumza Katibu Tawala wa Mkoa
wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi amezitaja fursa zinazopatikana
kwenye Mkoa huo kuwa ni pamoja na viwanda vya kuchakata mazao ya
mifugo,viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti na karanga,viwanda vya
kusindika asali,ranchi za mifugo na kilimo cha vitunguu. 

Vingine
ni viwanda vya kuchakata bidhaa za maziwa,viwanda vya kutengeneza
chakula cha samaki na mifugo,viwanda vya kutengeneza mvinyo,viwanda
kutengeneza jasi (gypsum),viwanda vya kuchakata korosho na uchimbaji wa
madini na mafuta

Aidha Mwenyekiti wa maonesho hayo Kanda ya Kati
Dkt. Mahenge alimwomba Mgeni Rasmi Mhe. Jafo kuiomba Serikali katika
mwaka ujao kufanyia maonesho ya Nanenane kitaifa katika viwanja vya
Nzuguni kwa kuwa ndiyo makao makuu ya nchi na kwamba uwanja huo
unakidhi vigezo vyote ambapo Mhe. Jaffo alikubali kuwasilisha ombili
hilo Serikalini.

Akifungua maonesho hayo ya Kanda ya Kati
Waziri Jaffo amewataka wananchi kutumia maarifa yanayotolewa na
wataalam ambapo amesema bado hayajatumika kikamilifu na kuagiza maafisa
ugani kote nchini kuhakikisha wanawasaidia wananchi kulima na kufuga
kisasa.

“Tuna fursa kubwa ya kujenga nchi yetu kwa kutegemea Kilimo, Mifugo na Uvuvi” amesisitiza Jaffo

Amepongeza
kuwa na paredi la mifugo kwenye maonesho ya mwaka huu na kuelekeza kila
Halmashauri nchini kuhakikisha inatenga maeneo ya kutosha ya malisho.

Aidha
amempongeza Katibu ya Kamati ya maandalizi ya maonesho hayo kanda ya
kati Bi Aziza Mumba ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia
Sekta ya Uchumi Mkoa wa Dodoma, pamoja na Kamati yake kwa maandalizi
mazuri ya mwaka huu ambapo ameitaka kamati hiyo kufanya maandalizi
mazuri zaidi katika miaka ijayo ili wananchi wanufaike zaidi na maarifa
yanayotolewa.

Bi. Mumba amesema Kamati yake imepokea na
itahakikisha kuwa inasimamia na kutekeleza maagizo hayo kikamilifu
ikiwa ni pamoja na kuboresha mapungufu yote yaliyojitokeza mwaka huu.

Mwaka
2020 ni mwaka wa kumi na tatu (13) katika kufanyika kwa maonesho ya
nanenane katika viwanja vya Nzuguni na ni mara ya Kumi (10) kuendelea
kufanya mashindano maalum ya paredi la mifugo ili kushindanisha mifugo
bora.